UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM SCHOOL OF LAW (SOL)

Tribute to the Late Hon. Justice NSEKELA H R December 2020

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

SHULE KUU YA SHERIA, CHUO KIKUU CHA DA ES SALAAM SALAMU ZA RAMBI RAMBI KWA KIFO CHA

JAJI HAROLD REGINALD NSEKELA TOKA KWA

EMERITUS PROFESSOR GAMALIEL MGONGO FIMBO

 

 

BWANA YESU ASIFIWE

Kwa unyenyekevu ninatoa pole kwa MKE na watoto wa Marehemu Jaji Harold Nsekela kwa msiba uliotokea katika familia. Vile vile ninampa pole mdogo wake VICAR, pamoja na ndugu wengine, jamaa marafiki na wale wote waliosoma na Marehemu au kufanya kazi naye.

Mini na marafiki zake watatu hivi tulikuwa tunamwita Jaji Harold.

Mimi nimesoma na Marehemu na nimekuwa mtu wa karibu sana naye. Nilikutana na Marehemu Jaji Harold tulipochaguliwa Kidato cha Tano (Form Five) TABORA BOYS SCHOOL mwaka 1963. Aliniambia kuwa darasa la 5 mpaka 8 alisoma Mpuguso Middle School, Rungwe.

Tulipomaliza Kidatu cha Sita (Form Six), Jaji Harold na mimi tulitunukiwa ufadhili (Fellowship) ya Rockerfeller Foundation ya miezi sita kupitia Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (University College Dar es Salaam). Msingi wake ni kuwa wafadhili wetu walibashiri sisi wawili tutafaulu vizuri mtihani wa Kidato cha Sita na hatimaye tutachaguliwa kusoma sheria.

Mpango wenyewe uliitwa Gap Project na tulitakiwa kuanza kujifunza mazingira na taratibu za mahakama. Jaji Harold alikwenda Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Tukuyu chini ya uangalizi wa Hakimu Mfawidhi (Senior Magistrate) Bw. S. K. Mshote. Mimi nilichagua Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya chini ya uangalizi wa Hakimu Mkazi Mfawidhi (Senor Resident Magistrate), Bw. R. H. Gilbert, kutoka Scotland.

Pale Mbeya nilifika tarehe 1 Januari, 1965 na nilipokelewa na baba mzazi wa Jaji Harold, Mwalimu Charles Nsekela ambaye alinitafutia chumba cha kupanga sehemu iliyoitwa Majengo. Wadogo zake wawili wa Jaji Harold, Geofrey (marehemu) na Vicar walikuwa wanasoma shule za msingi na kila mmoja alikuwa anaongoza kwenye mitihani shuleni kwake.

Jaji Harold na mimi tulianza masomo ya sheria (LL.B., Bachelor of Laws) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwezi Julai 1965; Mkuu wa Chuo akiwa Dr. Wilbert K. Chagula na Mkuu wa Kitivo cha Sheria akiwa Prof. A. B. Weston. Baada ya kufaulu mitihani ya mwisho, Jaji Harold, Jaji Thomas Leo Mkude (marehemu) na mimi tuliteuliwa kuwa Wakufunzi, (Tutorial Assistants). Miongoni mwa wanafunzi wa Jaji Harold mwaka ule ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Kenya, J. E. Gicheru, Jaji Mkuu Mstaafu wa Uganda, B. J. Odoki na Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Kenya,

S. A. Wako.

 

Cheo cha Tutorial Assistant kilitulazimu kuendelea na masomo ya juu. Jaji Harold alikwenda Marekani, Chuo Kikuu cha Yale (Yale University Law School), hali kadhalika Jaji Thomas alikwenda Marekani, Chuo Kikuu cha Columbia (Columbia University Law School), mimi nilikwenda Uingereza, Chuo Kikuu cha London (London University).

Aliporudi toka Marekani, Jaji Harold alichaguliwa kuwa Assistant Lecturer. Miongoni mwa wanafunzi wake ni Jaji Rufaa Wastaafu January Msoffe, William Mandia na Edward Rutakangwa. Mwaka 1972 Jaji Harold, akiwa na cheo cha Assistsnat Lecturer, alihamishia utumishi wake Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na mwaka uliofuata Jaji Thomas naye akiwa na cheo cha Assistant Lecturer, alihamia Tanzania Legal Corporation (TLC). Hapo TLC, Jaji Harold, Jaji Thomas na mimi mwenyewe hatimaye tulikutana kwa majukumu tofauti.

Jaji Thomas alipadishwa cheo kuwa Wakili Mkuu wa Shirika (Chief Corporation Counsel). Muda si mrefu baada ya mimi kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TLC mwaka 1983, Jaji Harold aliteuliwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Shirika (Deputy Chief Corporation Counsel).

Jaji Harold aliteuliwa kuwa Wakili Mkuu wa Shirika la TLC mwaka 1987 mara tu Jaji Thomas alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Sheria na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Miongoni mwa wanasheria ambao Jaji Harold aliowaongoza pale TLC ni Majaji Rufaa wastaafu Katherine Oriyo (Bibi) na Sauda Mjasiri (Bibi), Majaji wastaafu Regina Rweyemamu (Bibi) na Thomas B. Mihayo pamoja na Mawakili mashuhuri Dariah K. Bigeye (Bibi), Jotham Lukwaro na Julius Kalolo Bundala.

Nyota ya Jaji Harold iliendelea kung’ara: aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na baadaye Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Alipokuwa Jaji Rufaa, Jaji Harold alionyesha uhodari wake wa kuandika Hukumu za Mahakama (Judgment of the Court) kila aliposhiriki kwenye mashauri mbele ya Mahakama hiyo. Katika hukumu hizo, alidhihirisha umahiri wake kuwa alikuwa msomi wa sheria aliyebobea, mwerevu, mtenda haki, mwenye hekima na busara tele. Hakika, Jaji Harold ameacha hazina kubwa ya hukumu zinazowasaidia wanafunzi wa sheria, waalimu wa sheria, majaji na mahakimu katika kutekeleza majukumu yao.

Alipokuwa Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki (East African Court of Justice), Jaji Harold alifungua masjala za Mahakama hiyo kwenye Mahakama ya Rufani ya Tanzania hapa Dar es Salaam. Kwa kufanya hivi, aliwasaidia wananchi wenye nia ya kufungua mashauri katika Mahakama ya Afrika Mashariki.

Jaji Harold Nsekela, rafiki yangu, mwanafunzi mwenzangu, mwanataaluma mwenzangu, mwanasheria mwenzangu, Mmoravian mwenzangu, atakumbukwa kwa mengi.

BWANA ALITOA, NA BWANA AMETWAA,

JINA LA BWANA LIBARIKIWE, AMEN

Emeritus Professor Gamaliel Mgongo Fimbo, University of Dar es Salaam School of Law 7.12.2020.

 

 

Attachment: Download