UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM SCHOOL OF EDUCATION (SOED)

Announcements


CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM


HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM DHIDI YA MARADHI YA COVID19


Tangu kutangazwa kwa mwathirika wa kwanza wa maambukizi ya virusi vya korona (COVID-19) nchini Tanzania mnamo tarehe 16 Machi 2020, Serikali imechukua hatua kadhaa za kudhibiti kuenea kwa maradhi ya covid-19. Tunapenda kuwafahamisha wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na umma kwa ujumla kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeunga mkono juhudi za Serikali na wadau wengine katika kupambana na maambukizi ya virusi vya korona kwa kuchukua hatua muhimu zinazofafanuliwa hapa chini:
1. Kusanifu, kuunda na kusambaza mashine za kiotomatiki za kunawia mikono na zile zinazoendeshwa kwa kutumia miguu
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Kituo cha Maendeleo na Uhawilishaji wa Teknolojia (TDTC), kimeandaa aina mbili za mashine za kunawia mikono za kiotomatiki na zinazotumia miguu. Mashine hizi zina tanki la lita 250 na zimeandaliwa maalumu kwa ajili ya taasisi zinazohudumia idadi kubwa ya watu kama vile maeneo ya hospitali, viwanda na masoko. Mashine hizi zinatoa sabuni ya maji na maji baada ya mtu kusogeza mikono karibu na sensa kwa upande wa mashine za kiotomatiki na kukanyaga pedeli kwa upande wa mashine zinazoendeshwa kwa kutumia miguu. Mashine hizi ni nzuri na hazihitaji kufunguliwa kwa mikono hivyo kupunguza uwezekano wa kuambukizana kwa kushika mabomba ya maji. Aidha, Chuo tayari kimeshauza mashine hizi katika taasisi kadhaa zikiwemo, AMREF, BOT, NHIF, TAA, WFP, TOL, TAMISEMI, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na TANESCO.
Kama mchango wake kwa jamii, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia TDTC, kinatengeneza mashine 20 za kunawia mikono zitakazotolewa kama msaada kwa hospitali za Serikali zilizoandaliwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa COVID-19 jijini Dar es Salaam. Mashine zingine zitapelekwa katika vituo vikuu vya mabasi na daladala.
2. Uzalishaji wa barakoa za kiwango cha hali ya juu zenye matabaka matatu
Kitengo cha Vitambaa na Nguo cha Idara ya Uhandisi Mitambo na Viwanda

kikishirikiana na Kituo cha Maendeleo na Uhawilishaji wa Teknolojia (TDTC) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanza uzalishaji wa barakoa za kiwango cha hali ya juu zenye matabaka matatu. Uzalishaji huo wa barakoa ulianza kama hatua za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupambana na maradhi ya COVID-19. Barakoa hizo ni rahisi kutumia na zinaweza kutumiwa tena baada ya kufuliwa vizuri, kuua vijidudu kwa vipukusi na kunyooshwa. Malighafi za barakoa hizo ni hizi zifuatazo:
(i) Kitambaa cha nje (chenye rangi ya bluu) kilichofumwa kwa nyuzi za pamba chenye nyuzi za marefu zenye densiti ya 22/sm na nyuzi za mapana zenye densiti ya 19/sm
(ii) Kitambaa cha ndani (chenye rangi nyeupe) – kina nyuzi za marefu zenye densiti ya 45/sm na nyuzi za mapana zenye densiti ya 26/sm.
(iii) Kitambaa cha katikati ni chepesi hakijafumwa; kimetengenezwa kwa teknolojia ya spunbond.
Kila kitambaa kinazuia uingiaji wa erosoli (hewa yenye mchanganyiko wa dutu) yenye virusi vya korona, huku kitambaa cha katikati (kisichofumwa) kikisaidia kuchuja chembechembe za erosoli kutokana na muundo wa vitundu vyake vidogo vilivyobanwa vizuri.
3. Upimaji wa ubora wa barakoa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia vitengo vyake mbalimbali kimekamilisha utafiti wa ubora wa barakoa za vitambaa zinazozalishwa na taasisi na watu mbalimbali. Matokeo ya utafiti huo utakaotolewa hivi karibuni yameainisha aina mbalimbali za vitambaa vinavyotumika na ubora wake. Aidha utafiti huo umekuja na mapendekezo ya namna ya kutengeneza barakoa za vitambaa zenye ubora.
4. Uzalishaji wa Vipukusi vya Mikono (Vitakasa Mikono)
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanzisha mradi wa kuzalisha vipukusi vya mikono kwa ajili ya matumizi yake ya ndani na ya umma kwa ujumla. Taratibu za uzalishaji wa vipukusi hivyo vya mikono zimezingatia mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani ambapo, pamoja na viambata vingine, kunahitajika alkoholi isiyopungua asilimia 60.
HATUA NYINGINE ZINAZOCHUKULIWA
5. Kusanifu na Kuunda Mashine ya Umeme ya Kupumulia
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeanza usanifu wa kuunda mashine ya kupumulia. Hii ni mashine ya kiotomatiki inayowasaidia wagonjwa waliozidiwa kupumua.

UDSM Engineers fabricating special hand washing machines
6. Kuandaa Vyakula na Vinywaji vya Tibalishe Chuo Kikuu kimejiandaa kubaini, kupima na kuchanganua misombo na sumu katika bidhaa asilia zilizoteuliwa kama vile matunda, mbogamboga, mimea-tiba kwa ajili ya kuongeza virutubisho na kuandaa bidhaa za tibalishe. Lengo ni kuandaa antioksidanti, vizuia-mgando na vizuia-uvimbe asilia kwa ajili ya lishe bora na kujikinga na magonjwa.
7. Kutoa Fedha za Utafiti kuhusiana na ugonjwa wa Corona
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimewahimiza watafiti wake kuendelea kufanya tafiti kwa kasi zaidi ili kupata tiba, kinga au njia nyingine ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa corona. Kupitia Ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo – Utafiti, Chuo kimetenga fedha za utafiti na uvumbuzi kiasi cha Shilingi za Kitanzania 1,500,000,000/- (bilioni moja na milioni mia tano) katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 kwa ajili ya mapendekezo yanayohusu athari za maradhi ya COVID-19 na mada nyingine za utafiti. Chuo pia kimeanza kufanya utafiti wa tiba mbadala zinazoonesha uwezekano wa kuzuia au kupunguza makali ya COVID-19.
 

The University of Dar es Salaam Polarizing Microscope for testing the quality of face masks
University Ethanol Processing Facility (one of major ingredients needed for producing sanitizer)

Applied researches going on at the University of Dar es Salaam on the use of traditional medicine to treat different diseases including Corona associated symptoms
IMETOLEWA NA OFISI YA NAIBU MAKAMU MKUU WA CHUO - UTAFITI

Attachment: Download