UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
RESEARCH AND EDUCATION FOR DEMOCRACY IN TANZANIA (REDET)

Repoti ya Kiswahili ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2020

DIBAJI

Uchaguzi hutoa fursa kwa wananchi kuchagua viongozi au vyama wanaohudumu katika ofisi za umma. Ni njia muhimu ya kushughulikia ushindani wa kutafuta madaraka na utawala chini ya mfumo wa uliberali. Ni kitendo rasmi cha kufanya maamuzi ya pamoja ambayo yanajumuisha hatua kadhaa za msingi. Hatua hizo zinajumuisha kukubaliana kuhusu kanuni za mchezo, zikiwamo katiba, sheria na taratibu za uchaguzi, uteuzi wa wagombea, kampeni, upigaji kura, uhesabuji kura, utangazaji matokeo na mwisho kukubali au kukataa matokeo. Historia inaonesha kwamba mambo yanaweza kwenda kombo katika hatua yeyote kati ya hizi au katika hatua zote kwa makusudi au vinginevyo, na hivyo kufanya utazamaji uchaguzi kuwa ni shughuli muhimu.

Siasa za demokrasia ya kiliberali zilianzishwa tena barani Afrika mwanzoni mwa miaka ya 1990 zikitegemea sana utazamaji wa uchaguzi kama sehemu muhimu ya ustawi wake kutokana na sababu kuu tatu. Kwa kuanzia, kwenye nchi nyingi demokrasia ilianzishwa kwa msukumo wa nguvu za ndani na nje ya nchi. Haikua hiari au uamuzi tu wa kufanya hivyo. Ulikuwapo na bado kuna wasiwasi kuhusu uaminifu wa dola na vyombo vya kusimamia uchaguzi kutompendelea mtu yeyote. Hali kadhalika, kupitishwa na kuendelea kutumika kwa katiba za mfumo wa chama kimoja kulichangia wasiwasi huo. Katiba nyingi za aina hii zinaanzisha dola zenye nguvu dhidi ya mihimili mengine ya serikali na vyombo vya kusimamia uchaguzi ambavyo vinaonekana kukipendelea chama au mgombea fulani. Tatu, siasa za chama kimoja zinazokataza ukosoaji na zinazoviona vyama vya upinzani kama maadui ziliendelea. Vivyo hivyo, kuendelea kwa utamaduni wa kisiasa ambao unawaona raia kama watu wasiokuwa huru badala ya raia ambao wako huru ulikuwa kikwazo cha kuanzishwa kwa taasisi imara za kidemokrasia (Almond na Verba, 1963). Kwa ujumla, watu wengi walikuwa watiifu na waoga badala ya kuwa raia mahiri wanaojiamini na wanaotaka kutoa msukumo kwenye mfumo wa siasa (Mushi, 2001).

Kutokana na sababu hizo Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kupitia Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Kamati ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (TEMCO), iliamua kuendelea na utamaduni iliouanzisha wakati wa uchaguzi wa chama kimoja uliofanyika mwaka 1965 kwa kutafiti na kutazama uchaguzi wa kwanza uliofanyika chini ya mfumo wa vyama vingi mnamo mwaka 1995.

Je, utazamaji uchaguzi ulikuwa na umuhimu wowote miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi? Jibu lilikuwa ni ndiyo, hususan kwa sababu uimarishaji wa demokrasia nchini Tanzania haukuwa rahisi au mkamilifu kama ambavyo mtu mwingine angependa uwe. Katiba bado haina vipengele muhimu vya kidemokrasia. Na wakati huohuo jitihada za kuandika katiba mpya zimekwama tangu mwaka 2015 wakati Katiba Inayopendekezwa ilipopitishwa. Vyama vya siasa havijaimarika kiuendelevu. Kwa mfano, mafanikio makubwa vilivyoyapata katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yalifuatiwa na mlipuko ambao umeviacha vyama hivyo vimegawanyika na dhaifu, kama taarifa hii inavyoonesha. Uhuru wa kiraia na kisiasa si wa kudumu na unabanwa na sheria na kanuni nyingi mno. Uhuru huo unadhibitiwa na dola kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vingine. Chaguzi zilizopita hazikuwa huru na za haki. TEMCO ilionesha kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 ulikuwa huru lakini si wa haki, na chaguzi zilizofuata zilikuwa huru na za haki kiasi tu. Tanzania imefaulu jaribio la pili la Venezuela la mwaka 1992 ambalo linaonesha kwamba nchi inaimarika kidemokrasia kama inafanya chaguzi baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vyingi. Tanzania imeendesha chaguzi nne kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2020. Kwa maneno mengine, demokrasia ya mfumo wa vyama vingi imekuwapo kwa miaka 25. Kwa hiyo, Tanzania imefaulu jaribio la muda mrefu la Rustow (1970). Hakika, siasa za upinzani zimedumu muda mrefu. Hata hivyo, Tanzania haijawahi kushuhudia vyama vya siasa vikibadilishana madaraka.

Wanachama wamebadilishana uongozi ndani ya chama tawala. Hali ya kwamba chama tawala kinaweza kukubali kushindwa na kukabidhi madaraka kwa chama cha upinzani, kitu ambacho ni muhimu sana katika kuimarisha demokrasia, haijawahi kutokea (Huntington, 1991; Przeworski, 1991). Ni wazi kwamba jitihada za kuimarisha demokrasia nchini Tanzania bado zinaendelea, hivyo ni muhimu kuendelea kutazama mwenendo wa uchaguzi. Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ulipaswa kuwa mwepesi kwa sababu Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alikuwa anatetea kiti chake. Chama tawala kilihakikisha kwamba mgombea wake anapita bila kupingwa ndani ya chama, na hivyo kutekeleza kanuni ambayo haijaandikwa kwamba Rais aruhusiwe kugombea muhula wa pili bila kupingwa. Ukizingatia ugumu wa kawaida wa kumwondoa Rais aliyoko madarakani, watu walidhani kwamba ushindani na mwamko wa kisiasa ungekuwa mdogo. Hata hivyo, REDET iliona ni muhimu na lazima kutazama uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwani matumizi ya faida ya kuwa madarakani dhidi ya vyama vya upinzani yalikuwa makubwa.

Vitu viwili vilijitokeza kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Kwanza ni mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) ambao umeikumba dunia nzima, ikiwamo Tanzania. Lakini wasiwasi wa kwamba uchaguzi ungeweza kufanyika uliondolewa na Rais Magufuli mwanzoni mwa kipindi cha uchaguzi. Rais Magufuli alikataa kuweka zuio la watu kutoka nje kama jitihada za kupambana na janga hilo. Matokeo yake shughuli zote za kisiasa, kijamii na kiuchumi ziliendelea kama kawaida.

Pili, kutungwa kwa sheria mpya inayosimamia asasi zisizo za kiserikali, Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2019), kuliathiri zoezi la utazamaji uchaguzi. Mwaka 1995 TEMCO ilikuwa na wanachama 22. Idadi iliongezeka hadi 183 wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 unafanyika. TEMCO ilijumuisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS). Kifungu cha 2(b) cha sheria hiyo mpya, Sura 337, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 3 (2019), inakataza asasi za kidini kujishughulisha na shughuli za kisiasa. Hali hii iliinyima REDET/TEMCO michango ya watazamaji hawa wazoefu kutoka asasi za kidini. Hata hivyo, REDET ilitengeneza timu ya watu mahiri na waliojotoa kutazama uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Tunaomba kuwasilisha matokeo yao.

Profesa Rwekaza S. Mukandala

REDET/TEMCO

Mwenyekiti na Mkuu wa Timu ya Kutazama Uchaguzi

Tafadhali bonyeza ili kupakua repoti nzima

Attachment: Download