Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Rais Mstaafu Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ameridhika na kasi ya utekelezaji wa Mradi wa HEET katika Taasisi ya Sayansi ya Bahari ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo Zanzibar, huku akisema kuwa lengo la Chuo hicho baada ya ujenzi kukamilika ni kuwa kituo kikubwa cha Utafiti katika masuala ya Sayansi ya Bahari kwa Ukanda wa Afrika.
Dkt.Kikwete amesema hayo alipotembelea Taasisi ya Sayansi ya Bahari iliyopo eneo la Buyu Zanzibar hivi karibuni kukagua maendeleo ya mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET)ambapo katika Taasisi hii umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 11.
“Nimekuja kukagua ujenzi kuona tuko wapi; kwa mimi niliyekuja wakati ule kulipokua na msingi wa miaka 20 na niliyoyaona leo nimefurahi sana na nimefarijika kwamba kazi nzuri inaendelea kufanywa na ahadi iliyotolewa hadi kufikia mwezi wa 8 mwakani ambayo ni mwezi mmoja kabla ya muda wa mkataba, ujenzi unakamailika”, amesema.
“Kwa kinachofanyika hapa kama ilivyokua makusudi ya wakati ule ni kuwa kituo kikubwa cha Utafiti katika masuala ya Sayansi ya Bahari katika ukanda huu sidhani kama kuna kituo kikubwa kama hiki na mimi naamini tutakapokua tumekamilisha kwa maabara tutakazokua nazo,wakufunzi na wahadhiri watakaopatikana tutakijenga Chuo chetu kama kituo muhimu katika tafiti za bahari na viumbe hai”.
Dkt Kikwete ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Dkt. Hussein Mwinyi kwa kutoa kipaumbele kuhakikisha mradi huo unanufaisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu.