Na Zamda George, CMU
Kampuni ya ALAF Limited imeahidi kuendeleza ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambao umedumu kwa miaka sita sasa huku ikitangaza kutoa ufadhili wa masomo kwa baadhi ya wanafunzi wa Shahada ya Umahiri ya Kiswahili.
Hayo yameelezwa wakati wa hafla ya makabidhiano ya ufadhili huo wa masomo kwa wanafunzi wa Shahada ya Umahiri ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo ushirikiano huo umejikita katika kusaidia utoaji wa elimu ya juu nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa UDSM, watendaji wa ALAF Limited, wanafunzi, na wadau mbalimbali, Prof. Rose Upor, Rasi wa Ndaki ya Insia ambaye alimwakilisha Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Prof. Bonaventure Rutinwa, aliipongeza ALAF kwa kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya lugha ya Kiswahili kupitia ufadhili huo.
“Mpango huu umeleta matokeo chanya na kuunga jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuenzi na kutunza utamamaduni ambao unaambatana na lugha”, alisema Prof. Upor.
Ahadi ya kuendeleza Ufadhili
Naye Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa ALAF Limited, Bi. Hawa Bayumi, alisema Kampuni yake itaendelea kufadhili masomo ya wanafunzi wa Kiswahili kwa miaka ijayo.
“ALAF ni sehemu ya historia ya nchi hii, na tutaendelea kuwa sehemu ya jamii kwa kuwekeza kwenye elimu. Tunawapongeza wanafunzi walionufaika na ufadhili huu kwa juhudi zao na tunashukuru UDSM kwa ushirikiano wa muda mrefu”, alisema Bi. Bayumi.
Bi. Bayumi alieleza kuwa ALAF, iliyoanzishwa mwaka 1960 kabla ya uhuru wa Tanzania, ina historia ya kuhudumia jamii na imejikita katika kuendeleza sekta ya elimu kama sehemu ya dhamira yake ya kijamii.
Dkt. David Koloseni, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Shahada za Uzamili, Prof. Donatha Tibuhwa, alisema kuwa ufadhili wa ALAF umetoa mchango mkubwa katika uandishi wa insha na tafiti za Kiswahili.
"Wanufaika hawa wamekuwa chachu ya maendeleo ya Kiswahili, si tu kama walimu bali pia kama mabalozi wa lugha. Inapendeza kusikia Kiswahili fasaha kutoka kwao," alisema Dkt. Koloseni.
Wito kwa wanufaika
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Prof. Shani Omari Mchepange, aliwataka wanafunzi waliopokea ufadhili wa mwaka huu kujituma na kuwa mfano bora kwa wenzao.
"Tuna matarajio makubwa kuwa mtakuwa mabalozi wa Kiswahili na mfano wa kujituma na ubora wa kitaaluma," alisisitiza Prof. Shani.
Tangu kuanzishwa kwa ufadhili huo mwaka 2019, jumla ya wanafunzi 18 wamepokea ufadhili huo, huku baadhi yao wakiajiriwa katika taasisi mbalimbali za elimu kama vile Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Mmoja wa wanufaika wa awamu ya awali, Asha Silayo, alisema kuwa ufadhili wa ALAF umemsaidia sana kukamilisha masomo yake na kupata ajira ya kudumu katika sekta ya elimu. “Ni fursa isiyosahaulika”.
Miongoni mwa wanufaika wapya, Fredrick Venance amesema kuwa: "Najivunia kuwa sehemu ya mradi huu mkubwa. Nitahakikisha ninasoma kwa bidii na kuwa mfano bora wa kutumia lugha ya Kiswahili kwa usahihi na kutimiza ndoto zangu za kuendelea kielimu”.
Ushirikiano huu kati ya UDSM na ALAF ni muhimu sana katika kuboresha uhusiano uliopo kati ya sekta ya elimu na sekta binafsi katika kuendeleza taaluma, hasa Kiswahili, na hivyo, wadau wamesisitiza kuongezeka kwa idadi ya wanufaika kwa mwaka, na kufanikisha miradi mingine ya kielimu katika siku za usoni.