UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
COLLEGE OF HUMANITIES (COHU)

Salamu za rambirambi kufuatia kifo cha profesa Isaria Kimambo

SALAAM ZA RAMBIRAMBI KUTOKA KWA RASI WA NDAKI YA INSIA, DKT. ROSE A. UPOR, KUFUATIA KIFO CHA PROFESA ISARIA NDELAHIYOSA KIMAMBO KILICHOTOKEA TAREHE 2 NOVEMBA 2018, ITAKAYOSOMWA KATIKA UKUMBI WA NKRUMAH, CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM TAREHE 7 NOVEMBA 2018

 

Prof. Bonaventure Rutinwa, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taaluma;

Prof. Cuthbert Kimambo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Utafiti;

Dkt. Mussa Saddock, Mkuu wa Idara ya Historia;

Familia ya Marehemu Prof. Isaria Ndelahiyosa Kimambo;

Ndugu na Jamaa wa Marehemu Prof. Isaria Ndelahiyosa Kimambo;

Viongozi Waandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

Wafanyakazi na Wanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam;

Wawakilishi wa Taasisi na Makundi mbalimbali;

Mabibi na Mabwana;

 

Habari za Asubuhi.

 

Kwa heshima na taadhima na kwa niaba ya Ndaki ya Insia, ninaomba kuwasilisha salaam zetu za rambirambi kwa familia ya Prof. Isaria Ndelahiyosa Kimambo. Ni vigumu kuelezea simanzi iliyoipata Jumuia ya Ndaki ya Insia na hasa idara ya Historia. Taarifa za msiba huu mzito zilitufikia asubuhi ya tarehe 3 tukiwa kwenye maandalizi ya semina elekezi kwa ajili ya uongozi mpya ndani ya Ndaki ya Insia. Tulichukua muda kumtafakari shujaa wa taaluma ya Historia nchini kwa michango yake mingi na mikubwa sana hasa katika historia kama taaluma na historia kama somo linalofundishwa nchini.

 

Prof. Kimambo atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kujenga taaluma ya historia nchini kupitia machapisho yake lukuki pamoja na uongozi wake katika Chama cha Historia nchini, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Baraza la Mitihani la Tanzania. Kwa wale waliobahatika kufanya kazi enzi za uongozi wake wanamkumbuka kama kiongozi shupavu na mwenye uweledi wa hali ya juu. Kwa wengi wetu tulioajiriwa kipindi ambacho Profesa Kimambo alikuwa ameshastaafu, tunamkumbuka mwanazuoni mwenye maneno machache na sauti ya kiongozi, mwenye msukumo wa kujenga taaluma ya Historia na mwenye mapenzi ya dhati ya kuitumikia idara yake na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hata pale alipoonekana amechoka, hakutaka wanafunzi wake wakose usimamizi thabiti na idara yake ikose wahadhiri wenye weledi. Pale ambapo idara ya Historia ilionekana kukosa wahadhiri alijitoa kujaza nafasi hadi pale vijana wake waliokuwa katika masomo ya uzamivu waliporudi kushika hatamu. Tuna mengi tumejifunza kwa Prof. Kimambo na hakika tutaendelea kumuenzi kupitia mfululizo wa semina za kila wiki zinazofanyika katika Idara ya Historia. Hizi semina zimepewa jina lake, yaani Semina za Prof. Isaria Kimambo.

 

Tunawatakia safari njema wafiwa wote watakaomsindikiza Prof. Isaria Kimambo kwenye safari yake mwisho.

 

Bwana ametoa, na Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Roho ya Marehemu Prof. Kimambo ilale pema peponi.

 

Nimeombwa nimkaribishe Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Prof. Bonaventure Rutinwa aje atoe salaam za rambirambi kutoka kwa Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Karibu Prof. Rutinwa.