HOTUBA YA RASI WA NDAKI YA INSIA KWENYE UFUNGUZI WA SEMINA ELEKEZI YA VIONGOZI WAPYA WA NDAKI ILIYOFANYIKA UKUMBI WA COICT, KIJITONYAMA TAREHE 3 NOVEMBA 2018
Naibu Rasi wa Ndaki ya Insia, Dkt. Egidius Ichumbaki;
Wakuu wa Idara wapya katika Ndaki ya Insia;
Viongozi wa zamani wa Ndaki ya Insia;
Afisa Utawala wa Ndaki ya Insia, Bi. Dora Semkwiji;
Wafanyakazi wa Ndaki ya Insia;
Mabibi na Mabwana.
Habari za Asubuhi.
Siku ya leo ni siku ya kipekee kwa Ndaki yetu ya Insia kwa sababu ni kwa mara ya kwanza tunafanya semina elekezi ya uongozi mpya kwa miaka mitatu ijayo yaani 2018/19 – 2020/21. Hata hivyo, ni siku muhimu sana maana tumeukutanisha uongozi uliyopita na mpya katika ukumbi huu siku ya leo. Niseme kuwa ni fahari kubwa kwetu kama Ndaki na ni jambo la kujivunia maana tunapeana vijiti vya uongozi pasipo shaka na kwa imani kubwa kuwa yale yaliyofanywa na uongozi uliyopita, yataendelezwa na yataboreshwa uongozi mpya unaoingia.
Mabibi na Mabwana,
Kwanza nichukue fursa hii kuwashukuru wote mliyoitikia wito wa kukutana kwa lengo ya kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya kuiendesha Ndaki yetu. Mtakumbuka ya kwamba, tangu nimeingia kwenye uongozi mwaka 2017, kumekuwepo na mabadiliko kadhaa ya kiutendaji. Tumepokea wafanyakazi wapya na pia wafanyakazi wa zamani walihamishwa. Wapo wengine iliwalazimu kuachia nafasi zao kutokana na majukumu mapya yaliyojitokeza. Pamoja na hayo, mwanzo wa uongozi wangu ulijawa na mashaka na hofu nyingi baada ya Kiongozi aliyekuwepo awali kung’atuka pasipo kuwepo na maelezo ya kutosheleza. Zaidi ya yote, kulikuwepo na changamoto nyingi za kiutendaji na kiutekelezaji ambazo zilikosa maelezo ya kutosha ya kufanikisha uongozi ulioingia kupata msingi wa kufanya kazi. Ila hayo hayakunikatisha tama, maana jambo moja lilikuwa dhahiri, WanaNdaki ya Insia walikuwa na shauku ya mafanikio. Hilo lilinitosha kama msukumo wa kila nililofanya.
Ninapenda nichukue fursa hii kwa viongozi wanaomaliza muda wao, kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa namna walivyoniunga mkono tangu siku ya kwanza naingia ofisini. Haikuwa kazi rahisi kwa wao kufungua milango yao na kujenga imani katika maono niliyokuwa nayo kwa Ndaki yetu pendwa. Ikumbukwe ya kwamba, niliingia katika uongozi wa Ndaki baada ya kutokuwepo katika mazingira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kipindi cha miaka miwili. Hivyo nilikuwa ni mgeni kwa mambo mengi sana ndani ya Ndaki. Ninaomba mniunge mkono kwa kuwapigia makofi ya shukurani hawa viongozi wa zamani.
Mabibi na mabwana
Uongozi sio jambo rahisi sana kama ambavyo kila mmoja wetu angependa uwe. Uongozi unahitaji busara, usikivu, uvumilivu, uelewa, kujitoa, hisia, uaminifu, ukomavu na maumivu, mambo ambayo hayaandikwi kwenye barua za uteuzi. Maana kubwa ni kuwa uongozi unahitaji akili za kihisia yaani “Emotional Intelligence”. Kwa kawaida unapoingia katika uongozi, ni mara chache sana wale uliowakuta wakakupa mafunzo ya namna ya kuongoza kitengo ulichopewa na hata ukipewa mafunzo, yatakuwa mafunzo yanayotokana na changamoto iliyojitokeza na ambayo inahitaji usuluhishi papohapo.
Siku ya leo, menejimenti ya Ndaki, imeona ni vyema tutumie fedha zetu za ndani kwa manufaa yetu wenyewe kwa kujipatia mafunzo ya namna ambavyo tunapaswa kutekeleza majukumu yetu ili Ndaki yetu iweze kusonga mbele. Ninamshukuru Dkt. Raymond Boniface kwa kukubali wito wetu wa kuja kuzungumza na sisi juu ya mambo gani tunaweza tukajifunza katika uendeshaji wa taasisi kama ndaki yetu. Pamoja, naye yupo Dkt. Ichumbaki ambaye atatuongoza katika kuielewa Mpango Mkakati wa Ndaki ya Insia 2017/18 – 2021/22. Mpango Mkakati huu ni mwongozo wetu wa kufikia malengo ya kuwa Ndaki ya Insia inayoongoza Afrika Mashariki na Kati na pia Afrika kwa ujumla. Bi Dora Semkwiji atazungumza kuhusu majukumu ya wafanyakazi waendeshaji. Na kama mnavyoona, waalikwa wetu leo ni pamoja na wafanyakazi waendeshaji maana wao ni kiungo muhimu sana katika kufikia mafanikio. Bila wao Ndaki, ni sawa na gari lisilo na mwendeshaji.
Napenda nisisitize kuwa semina hii itaongelea mambo muhimu sana ambayo yatahusisha wafanyakazi wa kada zote, maana utekelezaji wa majukumu katika Ndaki sio ya kitaaluma pekee ni pamoja na uendeshaji. Hivyo, niwaase tuwasikilize kwa makini yale yatakayowasilishwa kwetu leo. Na nisisitize kuwa yasibaki kuwa ni historia kwetu, bali tukitoka hapa twende tukayaishi mafunzo haya katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku. Ni vyema muelewe kuwa sisi sote tuliopo humu ndani ni sawa na mfumo wa mashine ulio na vipuri vingi/sehemu nyingi. Ili mfumo uweze kufanya kazi vizuri, kila sehemu inabidi ifanye kazi kufuatana na hitaji iliyopo. Pale ambapo sehemu katika mfumo utalega au itakuwa mbovu basi mfumo mzima hautafanya kazi, hivyo kukosekana kwa mafanikio. Katika lugha rahisi, sisi sote ni muhimu sana katika Ndaki ya Insia kufikia malengo yake na mfanikio makubwa.
Mabibi na Mabwana
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita nikiwa na uongozi wa zamani, tuliweza kufikia mafanikio mengi sana. Ningependa kutaja machache kwa wale pengine hawakupata fursa ya kuyafahamu.
Haya ni machache ambayo naweza kutaja kwa haraka sana ila kuna mengi sana pengine tungeweza kujaza kurasa. Niseme tena Asante kwa viongozi wetu maana bila wao, mafanikio haya yasingepatikana. Nisije kuwa mchoyo wa fadhila pia kwa viongozi wengine wa zamani ambao tunaendelea kuwa pamoja nao katika kipindi hiki. Naomba tuwashukuru na wao maana bado wana imani ya kuwa huko tunakoelekea kama Ndaki, kuna mafanikio na wasingependa kuachwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo.
Mabibi na Mabwana
Nimetumia muda kidogo kuonyesha shukurani zangu kwa viongozi wa zamani ila sijawaeleza kwa nini nimewaalika hapa kwa niaba ya wanaNdaki. Sababu kubwa ya kuwaalika viongozi hawa ni kusema ASANTE. Mara nyingi wengi tukifanyiwa jambo kibinadamu tunakuwa wepesi wa kusahau yale waliyoyapitia ilikufanikisha kile tulichokihitaji kwa wakati huo. Tulihitaji uongozi, wakatupa, tulihitaji usikivu wao, wakatusikiliza, tulihitaji utendaji wao, wakafanya, je ni vyema tuwaache waondoke pasipo kuwaambia Asante? Hatuna kikubwa sana ya kuwapa zaidi ya kuwatambua kwa utumishi wenu uliotukuka. Kumbukeni kuwa Ndaki yetu ni changa, yaani ina miaka 4 tu tangu kuanzishwa kwake, na nyie mliipa thamani ambayo haitasahaulika katika historia ya Ndaki hii. Ninaomba msimame tuwatambue kwa makofi mengi.
Mabibi na Mabwana
Nisiwachoshe kwa hotuba ndefu sana. Ila mniruhusu kuchukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa kamati ya maandalizi ya semina hii. Naomba tutambue mchango ya wafuatao, Bi Dora Semkwiji, Bw. Arnold Bitegeko, Bw. Vedastus Bakari, Bi. Pudensiana Msuya na Bw. Kibugila. Nisisahau ofisi ya mapokezi kwa jitihada walizoweka pia katika kufanikisha baadhi ya shughuli za maandalizi ya semina hii. Napenda pia niishukuru Ofisi ya Naibu Makamu mkuu wa Chuo- Utawala kwa kutuwezesha kupata vibali mbalimbali.
Ni matumaini yangu semina elekezi zitaendelezwa katika historia ya Ndaki na hii itatunzwa katika kumbukumbu za ndaki. Kwa maneno machache naomba nitangaze Semina Elekezi imefunguliwa rasmi.
Asanteni.