Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinapenda kuutarifu umma kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ataweka jiwe la msingi la jengo la Taaluma na Utawala (awamu ya pili) katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Buyu, Zanzibar tarehe 5 Januari 2025 saa 2 asubuhi. Hafla hili ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Ujenzi wa jengo hilo ni miongoni mwa shughuli za utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation-HEET) unaotekelezwa kwa mkopo masharti nafuu wa Benki ya Dunia kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kupitia mradi huu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kuzingatia mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
Bajeti iliyotengwa kwa shughuli za ujenzi IMS, ni Shilingi Bilioni 11 ikijumuisha jengo lenye maabara tano zenye uwezo wanafunzi 114 kwa wakati mmoja; madarasa 10 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 kwa wakati mmoja; ukumbi wa kisasa wa mikutano kwa watu 150; na ofisi 41 za wafanyakazi zaidi ya 80. Vilevile, mradi unafadhili ujenzi wa bweni la wanafunzi 40.
Hafla hii ni fursa adhimu kwa wananchi wote kushuhudia hatua muhimu ya uwekezaji wa Serikali katika elimu ya juu, hasa katika sekta ya uchumi wa buluu, ambayo inachangia kiasi kikubwa katika maendeleo endelevu Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinawakaribisha wananchi wote na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika tukio hili la kihistoria na katika kuunga mkono Kaulimbiu ya Mapinduzi: Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo ya Taifa.
Mapinduzi Daima!
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
04 Januari 2025