Lugha Kiswahili Yaendelea Kupata Msukumo Kimataifa: UDSM Yajizatiti Duniani katika Fasihi, Elimu na Utamaduni
Na Jackson Isdory, CMU
Katika mwendelezo wa Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASIKIDU) mwaka 2025, Kiswahili kimeendelea kupewa msukumo katika jukwaa la kimataifa kupitia ushirikiano wa kimkakati kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), taasisi za kitaifa na kimataifa, na wadau wa sekta binafsi.
Hili limejidhihirisha kupitia matukio makuu mawili yaliyofanyika UDSM, Tanzania na Chuo Kikuu cha Taaluma za Kigeni cha Beijing (BFSU), China, yakionyesha namna Kiswahili kinavyoendelea kuwa nyenzo ya maarifa, utambulisho na diplomasia ya kitamaduni.
Matukio hayo ni pamoja na hafla ya tuzo za Safal na uzinduzi wa wa maadhimisho ya miaka 100 ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).
Tarehe 3 Julai 2025, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kilifanya hafla rasmi ya utoaji wa Tuzo ya Safal ya Fasihi ya Kiafrika, sambamba na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 100 ya Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), ambapo Mgeni rasmi, alikua Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb).
Waziri Prof. Kabudi alisisitiza kuwa Kiswahili ni chombo cha kuakisi historia, maadili, na maendeleo ya jamii pamoja na kuwa nyenzo ya kujenga jamii inayojifaharisha na utamaduni wake, yenye mshikamano na inayojitambua.
“Kiswahili si tu lugha ya mawasiliano bali ni “silaha ya kiutamaduni, elimu, na maendeleo”. Kuna umuhimu wa kuwekeza katika tafsiri, uandishi, na matumizi ya Kiswahili katika elimu na utawala, huku akitoa wito kwa TATAKI kuwa kitovu cha harakati za kufanikisha Kiswahili kuwa lugha ya umoja wa Afrika”, amesema Prof. Kabudi.
Akizungumza kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utafiti, Prof. Nelson Boniface, alieleza: “Ushirikiano wetu na Safal Group unaonesha dhamira ya dhati ya kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa njia ya maarifa, ubunifu na ajira. TATAKI ni taasisi ya kihistoria barani Afrika yenye mchango mkubwa katika sera za lugha.”
Kwa upande wa Safal Group, Afisa Mkuu wa Masoko, Mawasiliano na Mahusiano ya Nje, Bw. Anthony Ng’ang’a, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji Bw. Anders Lindgren, alieleza dhamira ya kampuni yao katika kuunga mkono miradi yenye athari chanya katika jamii.
“Safal Group tunaamini kuwa maendeleo ya jamii hayawezi kutenganishwa na maendeleo ya utamaduni. Lugha ni daraja kati ya kizazi cha sasa na kizazi cha kesho. Tumewekeza katika Tuzo ya Fasihi ili kutoa jukwaa kwa sauti za Kiafrika kusikika duniani,” alisema Bw. Ng’ang’a.
Katika kuchochea uvumbuzi na ubunifu kupitia lugha ya Kiswahili, ALAF, kampuni tanzu ya Safal Group, imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia utoaji wa tuzo hizi kwa miaka tisa mfululizo.
Mkurugenzi Mkuu wa ALAF, Bw. Ashish Mistry, alisema kuwa “Uwekezaji wetu katika lugha ya Kiswahili ni wa kimkakati. Tunaamini Kiswahili ni kichocheo cha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi. Tunapowasaidia wanafunzi, waandishi na wataalamu wa lugha, tunachangia moja kwa moja kwenye ajenda ya maendeleo ya taifa letu.”
Beijing Yasema Ndiyo: Kiswahili Kimefika Mashariki ya Mbali
Wakati huohuo, ili kuonesha namna Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinavyokiheshimisha Kiswahili kwa kufundisha, kuendeleza, kutafiti na kukieneza duniani kote, tarehe 8 Juni 2025, wataalamu wa UDSM walishawishi Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU), kwa ushirikiano na Shirika la Uchapishaji la SHITU, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuratibu maadhimisho ya kihistoria yaliyoambatana na mashindano ya kitaifa ya hotuba na hadithi kwa Kiswahili.
Hafla hiyo, iliyoambatana na sanaa za maonyesho, iliwakutanisha wanafunzi kutoka vyuo saba vya China vinavyofundisha Kiswahili.
Akihutubia kama mgeni rasmi, Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar, alieleza kuwa Kiswahili ni urithi hai wa Afrika unaopata heshima kubwa duniani. “Kuwapo kwa Kiswahili katika muktadha wa kimataifa ni ushahidi wa nguvu ya lugha kama zana ya diplomasia ya kitamaduni”.
Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha BFSU, Prof. Zhao Gang, alieleza kuwa zaidi ya wanafunzi 200 wamehitimu katika taaluma ya Kiswahili tangu mwaka 1961 na kwamba lugha hiyo sasa ni miongoni mwa lugha 20 za Kiafrika zinazofundishwa chuoni hapo.
Katika hafla hiyo ya MASIKUDU huko Uchina, wanafunzi waliwasilisha hoja kwa ustadi wa hali ya juu, wakizungumzia ushawishi wa Kiswahili katika uhusiano wa China na Afrika, na umahiri wao wa hadithi ulizua msisimko wa kihistoria.
Majaji mashuhuri akiwemo Prof. Shani Omari wa UDSM anayetumia likizo yake ya kunoa ubongo katika Chuo Kikuu cha BFSU, Bi. Consolata Mushi ambaye ni Katibu Mtendaji wa BAKITA na Pamela Ngugi walisisitiza kiwango cha ubora na ujasiri kilichoonyeshwa na washiriki.
Prof. Shani Omari, aliyeiwakilisha UDSM, alieleza kuwa mafanikio ya tukio hilo ni ushahidi wa mafanikio ya mkakati wa kimataifa wa kukuza Kiswahili “Kiswahili hazikibani lugha nyingine kama baadhi ya watu wanavyodhani bali kinazikumbatia na kuzitumia kama hazina muhimu, ndio maana kinafaa kuwa lugha ya Umoja wa Afrika.”
Dira ya Kiswahili: Ajira, Biashara na Ushirikiano wa Kimataifa
Kwa kuzingatia mchango wa taasisi za elimu kama TATAKI, kampuni binafsi kama Safal na ALAF, na ushirikiano wa mashirika ya serikali kama BAKITA, ujumbe unaojitokeza wazi ni kuwa Kiswahili sasa si suala la kitaifa pekee, bali ni fursa katika uga wa maendeleo kimataifa.
Ushirikiano huu wa kimkakati unahitaji kuendelezwa kwa njia ya mikakati kabambe ya kufundisha Kiswahili, kuandika fasihi, kutoa tafsiri, kuanzisha maktaba za kidijitali, na kushirikiana na taasisi kama UNESCO, CODESRIA, ALAF na Baraza la Kiuchumi la Kijamii na Utamaduni la Umoja wa Afrika (ECOSOCC).
Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili UDSM (TATAKI), Prof. Aldin Mutembei alisema: “Tuna wajibu wa kuandaa kizazi cha walimu, waandishi na wakalimani wa Kiswahili. Kiswahili ni fursa ya ajira, biashara, na utangamano wa Bara la Afrika.”
Pia Prof. Mutembei alitoa wito kwa wanafunzi wa Kiswahili kuwa na weledi katika lugha fasaha na pia kujifunza lugha za kimataifa ili kuchangamkia fursa za ukalimani, tafsiri na diplomasia ya lugha.
Katika warsha maalum iliyoandaliwa kwa wanahabari na watunzi wa tamthiliya, Mkurugenzi mwenza wa Taasisi ya Conficius, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Mussa Hans aliwahimiza waandishi wa habari kutumia Kiswahili sanifu huku wakihakikisha kwamba wanatumia kamusi kama sehemu ya marejeleo muhimu na kuomba msaada wa kitaaluma pale inapobidia.
Akieleza kuhusu ushirikiano baina ya UDSM na sekta binafsi, Dkt Hans alisema: “Ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Safal Group ni wa kihistoria na ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano baina ya taaluma na sekta binafsi. Kampuni ya ALAF kupitia Safal Group imekuwa ikifadhili wanafunzi wa Kiswahili na kusaidia kukuza vipaji vya uandishi na fasihi ya Kiafrika.”
Mustakabali wa Kimkakati: Kiswahili ni Sera ya Maendeleo
Prof. Kabudi alisisitiza kuwa: “Kiswahili ni chetu. Kiswahili ni cha Afrika. Kiswahili ni cha dunia. Maadhimisho haya si mwisho, ni mwanzo wa enzi mpya ya Kiswahili duniani”.
Kwa kuenzi usemi wa Kiswahili usemao “Kiswahili ni mali, akilimaye hulisha,” mataifa ya Afrika na washirika wake duniani wanapaswa kuendelea kuwekeza katika lugha hii kwa njia ya sera, elimu, teknolojia, na ushirikiano wa kimataifa.
Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani si sherehe tu, ni jukwaa la kimkakati la kuandika historia mpya ya Afrika. Kwa mtazamo wa kimkakati, maadhimisho haya yanapaswa kutazamwa kama kipimo cha nguvu tepe ya lugha, ushawishi wa Afrika katika medani ya kimataifa, na nafasi ya lugha ya Kiswahili katika diplomasia ya kiuchumi.
Ni fursa kwa taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi, na serikali kufanya kazi kwa pamoja ili Kiswahili kiwe si tu lugha ya kuzungumzwa, bali pia kiwe lugha ya kufikiri, kuongoza, na kuleta mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiutamaduni duniani.