Skip to main content
Body

Salamu za Pole

Mkuu wa Chuo, Baraza, Menejimenti na Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) tumepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Jaji Mstaafu Julie Catherine Manning kilichotokea tarehe 20 Machi 2026 katika Kituo cha Afya cha Hitech Sai, Upanga, jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.

Jaji Julie Catherine Manning alizaliwa tarehe 24 Januari 1939 Mkoani Morogoro. Safari yake ya elimu ilianzia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Tabora kabla ya kujiunga na Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kikiwa Chuo Kishiriki cha Chuo Kikuu cha London, Uingereza) mwaka 1961. Alikuwa mwanafunzi pekee wa kike miongoni wa wanafunzi 14 wa kwanza kabisa chuoni hapa, na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Tanganyika na Afrika Mashariki kusomea taaluma ya sheria katika chuo hiki.

Jaji Manning alihitimu Digrii ya Sheria mwezi Agosti mwaka 1964, akiwa miongoni mwa wahitimu 12 wa kwanza katika mahafali ya mwanzo kabisa katika Chuo hiki. Alianza kazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama mtaalamu wa uandishi wa sheria, akiwa mwanamke wa kwanza nchini kushika nafasi hiyo katika kipindi ambacho taaluma ya sheria ilikuwa ikitawaliwa zaidi na wanaume.

Mwaka 1973, aliteuliwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kushika wadhifa huo. Uteuzi huo uliashiria hatua muhimu katika historia ya maendeleo ya wanawake katika uongozi na taaluma ya sheria nchini na kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Soma Zaidi >

Announcement Date