KONGAMANO KUHUSU HALI YA UNCHUMI NA SIASA NCHINI TANZANIA 1 NOVEMBA 2018


KONGAMANO KUHUSU HALI YA UCHUMI NA SIASA NCHINI TANZANIA TAREHE 1 NOVEMBA 2018

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimefanya Kongamano Kuhusu Hali ya Uchumi na Siasa Nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitatu (3) ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu aingie madarakani tarehe 05.11.2015. Kongamano hilo lilifanyika mnamo tarehe 01.11.2018 katika Ukumbi wa Nkrumah, Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, Mlimani.

 

Katika kongamano hilo, wasomi mbalimbali walipata nafasi ya kuchambua utendaji wa Serikali ya awamu ya tano juu ya namna Serikali ilivyochukua hatua mbalimbali za kuboresha uchumi, huduma za jamii, upatikanaji wa nishati, miundombinu, kuinua sekta ya viwanda, kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma, kuongeza nidhamu katika utumishi wa umma, kupambana na rushwa, na kuongeza uwajibikaji.

 

Katika uchambuzi huo, wasomi walijikita katika mada kuu Tano ambazo ndizo zilitawala mjadala husika. Mada hizo ni “Hali ya Uchumi na Maendeleo ya Viwanda” iliyowasilishwa na Profesa Humphrey Moshi wa Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; “Nishati na Miundombinu” iliyowasilishwa na Profesa Hudson Nkotagu   wa Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; “Lugha na Maendeleo” iliyowasilishwa na Profesa Martha Qorro wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; “Huduma za Jamii” iliyowasilishwa na Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni Katibu Mkuu, Wizara ya Maji; na “Hali ya Siasa na Utawala” iliyowasilishwa na Profesa Rwekaza Mukandala wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

 

Akihitimisha mjadala huo, Prof. Rwekaza Mkandara amemfananisha Rais Magufuli na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa nia, mawazo na vitendo kwamba Mwalimu Nyerere alikemea ukupe na rushwa na Rais Magufuli anakemea majipu na kuyatumbua; Mwalimu Nyerere alikuja na "Uhuru na kazi", Rais Magufuli kaja na "Hapa kazi tu, asiyefanya kazi na asile"; na Mwalimu Nyerere alikuja na "Uhuru na maendeleo", na Rais Magufuli kaja na "Tanzania ya Viwanda".

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Mgeni Mshiriki Maalum wa Kongamano hilo aliwashukuru wasomi hao kwa kumwalika na aliwapongeza wawasilisha mada na wachangiaji wote kwa umahiri waliouonesha kwa kuchambua mada husika mbele yake bila hofu na mashaka, ila kwa ujasiri mkubwa na kuonesha hali halisi ilivyo katika serikali yake. "Serikali yangu imepokea ushauri na maoni kama yalivyotolewa na tutayatekeleza kama yalivyo", aliahidi Rais Magufuli alipopewa nafasi ya kusalimia wana kongamano hao. "Nialikeni tena, nitakuja", aliongeza Rais Magufuli.

 

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, kina wajibu wao kutathmini serikali iliyopo madarakani ili kutoa maoni ya kitaalam na ushauri juu ya namna bora ya kuendesha mambo mbalimbali bila kuwaumiza wananchi wa Tanzania na dunia kwa ujumla.